MAAJABU YA AKIBA

SIMULIZI YA KUFURAHISHA,
“KUHUSU HATIMA YA KIMUNGU”.
SEHEMU YA NNE.
Elvine alishituka na akajikuta hospitali.
Alishangaa kuona kazungukwa na watu asiowajua kabisa, na cha ajabu
zaidi walikuwa ni wachina wanne na mwafrika mmoja. Aliogopa sana kisha akauliza
"hapa ni wapi?". Watu wale walionyesha tabasamu lililoashiria furaha
ya yeye kuamka, lakini walionesha kuwa hawakuwa wanamuelewa kabisa
anachoongea....
Kupata sehemu iliyopita bonyeza hapa
Sasa inaendelea.....
Elvine alizidi kuogopa baada ya kuchomwa sindano ambayo ilimfanya ahisi kuishiwa nguvu, kisha macho yake yakalegea na mwisho yakafumba kabisa. Alishituka badae na kujikuta kitandani, tena kwenye nyumba ya kifahari mno. Hakuwa anajielewa vizuri, aliamua kutoka nje. Alipofika sebuleni, alikutana na sebule nzuri mno ambayo hakuwahi kuona kwa macho toka azaliwe zaidi ya kwenye sinema tu.
"Mmmh! hapa
ni ulaya nini?" Alijihoji huku akiwa haamini. Alisogea mbele kidogo, ghafla
alikuja mama mmoja ambaye ni chotara wa kizungu na kichina na alikuwa akiitwa
Exhao Mke wa Mr. Ezhu yang , yule mama na akasema "ooh! my
son. How do you feel now?. Am proud you are good now."(ooh! Kijana wangu unajisikiaje sasa?. Najivunia upo vizuri Sasa)". Elvine alimkodolea macho
tu yule mama pasipo kujibu neno, maana hakuwa anaelewa kitu, zaidi
alichoelewa ni "my son" tu! Lenye maana ya kijana
wangu, kitu
kilichomfanya asielewe zaidi ni rafudhi na uongeaji wa haraka wa yule mama.
Elvine alizidi kupata hofu
maana hakujua yuko wapi, na yule mama ni nani. Yule mama na Elvine hawakuwa
wanaelewana kabisa maana kila mmoja alitumia lugha anayoielewa yeye.
Yule mama akaamua kumshika mkono Elvine
hadi mezani ambako kulikuwa na vyakula vingi mno
kana kwamba kuna sherehe pale ndani. Dakika chache baadaye wakiwa pale mezani,
alikuja baba mmoja wa kichina na kukaa kitako mezani huku akiwa na furaha mno,
"unakwendeleaje?"
"Vizuri" alijibu Elvine maana
alimuelewa japo hakuwa anajua kiswahili vizuri baba yule.
"Unajionaje afya jako sasa?, Moyo jangu
ulipasuka pasuka baada ya kukuta hali
yakyo ni mbaya" alihoji mchina yule huku akiwa na kiswahili cha kipekee
kidogo, lakini haikumpa shida sana Elvine kumuelewa. Kwahiyo akamjibu kuwa yeye
hali yake ni njema.
Elvine moyoni mwake alikuwa na shauku kubwa
sana ya kumwona mama yake hivyo aliamua kuuliza kuwa ni nini kimetokea
na yuko wapi mama yake Editrin, lakini yule baba alisema
wale kwanza halafu atamwambia siku nyingine kuhusu hilo.
Elvine alipewa uma na kisu, na mezani
kulikuwa na nyama za kila aina, tambi, wali na vingine vingi ambavyo yeye
hakuvijua.
Alipeleka mkono kwenye tambi na akajichotea
na kuanza kula, lakini sasa, loo! Radha aliyoitegemea haikuwa yenyewe kabisa
lakini alijikaza na akala vijiko viwili tu, aliitamani nyama lakini staili ya
ulaji wa wale watu ilimtisha maana kwao hawajawahi kula na kisu wala uma nyama, bali ni mikono tu ndiyo ilikuwa
ikifanya kazi yake.
Aliamua kuugeukia wali lakini pia hapakuwa na
kijiko pale mezani, lakini akajipa moyo mkuu, maana njaa ilkuwa
kali sana. Alijitahidi kuula wali ule kwa uma na akaweza. Mwishoni mwa chakula
akaona haina haja ya kujitesa wakati yeye ni mpenzi wa
nyama, aliamua
kutumia mkono wake, na akala pande moja la
kitimoto
lililonona haswaa!. Wale watu walimtazama tu na wakaonekana
kufurahia hata alichokifanya.
"Ooh dear, poye kwakua
hatukuchua kuwa hujajua kuitumiya hiyi kishu
na umaa"
Elvine alitabasamu tu na hakujibu neno lakini alitamani kucheka, ila heshima tu ndiyo ilimzuia. Baada ya kula aliondoka
mezani na kurudi chumbani alikokuwa kalala mwanzo. Kichwani alikuwa na
maswali mengi sana ambayo yalihitaji ufafanuzi lakini hakujua aanze kumuuliza
nani pale ndani.
Akiwa chumbani alijikuta anaanza kulia huku
akitaja 'mama', maana alihisi woga
kidogo hasa kukutana na watu ambao hawajui kabisa.
Ghafla mlango ulifunguliwa na wakaingia
mabinti wawili na kijana mmoja wenye umri wake pamoja na yule baba wa kichina.
Walipoingia Elvine kwa woga alishituka sana, akakurupuka pale kitandani na
kusimama karibu nao. Yule baba akasema kuwa yeye anaitwa Mr. Ezhu yang na ni
mchina lakini anafahamu kiswahili kidogo maana aliwahi kukaa
Tanzania kama mwaka na miezi minne akiwa katika "research" ya
kisayansi kabla hajafungua hospitali yake, na kuhusu mama yake asijali yupo tu.
Lakini pia alimwambia pale ni Shanghai nchini
China hivyo asihofu kabisa. Na wale watoto aliokuja
nao ni marafiki zake kwanzia sasa maana ni watanzania ambao watamsaidia sana
yeye kujua kiingereza vizuri na kuyazoea mazingira . Yule baba baada ya kuongea
hayo aliondoka na kuwaacha wale mabinti wawili na kijana mmoja.
Binti mmoja alimsogelea Elvine na
kumsalimia.
"Habari yako!"
"Njema"
"Sisi ni watanzania kama wewe,
hapa tupo kimasomo tu, lakini pia sisi tunajua kiingereza na kichina kidogo,
maana toka tukiwa wadogo tumesoma huku. Kwani kule
unakaa sehemu gani?.
Kabla Elvine hajajibu na yeye akamuuliza yule binti swali.
"Hivi tumeshawahi kuonana
mahali? Maana sura yako sio ngeni kwangu"
"Sina uhakika, ila mimi sizani".
Kabla hawajaendelea kuulizana maswali yule binti simu yake iliita na
alipoipokea aliongea kiingereza kama mzungu wa marekani. Elvine alipata kawivu
kidogo na akatamani sana angekuwa yeye. Yule binti baada
ya kumaliza kuongea na simu aliondoka na akasema kaitwa nyumbani ila atakuja
tena kesho kumuona. Baada ya yule binti kuaga na wale wenzake pia
wakasema wanaondoka
Elvine alibaki pale akiwa hajui hatima yake.
Rafiki zake wale, wakiafrika walizidi kuja
siku baada ya siku hivyo akawazoea sana, lakini hakuruhusiwa kutoka pale ndani
kwaajili ya matembezi wakidai bado ni mgeni. Baada ya miezi minne
kupita alianza kujua vizuri kiingereza
maana kila mtu alikuwa anaongea kiingereza na kichina tu mule ndani na hata Mr.
Ezhu hakuwa mtaalamu wa kiswahili. Baada ya kuanza kuelewa
kiingereza alipelekwa shule ya kimataifa iliyopo pale
Shanghai.
Hakuwa anaelewa chochote maana yeye aliishi kwa maelekezo tu
kutoka kwa Mr. Ezhu yang. Alikaa kwa muda na akaanza kufurahia maisha ya pale,
hasa baada ya kujua kiingereza.
Siku moja usiku aliota mama yake anamuita
huku analia sana. Baada ya ndoto ile alianza kuona
kuna umuhimu wa yeye kujua kwanini mama yake hayupo pamoja naye.
Alianza kuwasumbua walezi wake yaani, Mr Ezhu yang na mkewe madam Exhao.
Siku moja akiwa chumbani kwake, alikuja
daktari ambaye alijitambulisha kwa jina la dokta Exqu xhiao na alikuja na nesi
wa kizungu aliyeitwa nesi Emma. Walimchoma sindano
mkononi huku
wakisema kuwa ni kwaajili ya afya yake maana bado hajapona vizuri.
Baada ya ile sindano kuingia mwilini na
kusambaa vizuri alianza kuhisi maumivu ya kichwa. Ghafla
aliingia yule mama wa kizungu ambaye ndiye alikuwa wakwanza kumuona baada ya
kuingia kwenye nyumba ile. Na alionekana kuwa na hasira sana
"This is not ok! (Hii sio sawa)".
Yule mama alifoka kwa jaziba sana. Kisha alianza kugombana na wale watu kwa
kichina, kwahiyo hakuna ambacho Elvine alielewa
baada ya lile jambo. Wakati ugomvi unaendelea aliingia Mr. Ezhu yang na
akimshika mkewe kwa nguvu na kutoka nae nje.
"It's ok baby" (usijali mtoto).
Alisema yule daktari huku akimshika kichwa Elvine na kuchezea
nywele zake. Elvine hakuwa anaelewa chochote, alichomwa sindano nyingine na
hapo ndipo alipoishiwa nguvu kabisa na kulala.
Huku nje Mr. Ezhu yang alikuwa katika
mgogoro mkubwa na mkewe. Mgogoro wao ulikuwa katika uamuzi wa Mr. Ezhu kuamua
kumfuta yule mtoto kumbukumbu jambo ambalo Exhao hakuridhia kabisa.
Mr. Ezhu aliondoka kwa hasira pale ndani.
Wakati Exhao akiwa hajui cha kufanya alienda chumbani kwao na akawa anakumbuka
namna walivyompata Elvine.
Alikumbuka kuwa miezi michache iliyopita
yeye na mumewe walikuwa Tanzania katika matembezi. Exhao hakubahatika
kuwa na mtoto toka aolewe na Mr. Ezhu yang hivyo alitamani hata kulea mtoto
yeyote kutoka katika kituo cha watoto yatima.
Siku moja usiku alikuwa kwenye gari yeye na mumewe,
wakiwa wanatoka kufanya utalii wao katika hifadhi ya kituro baada ya kuchelewa
sana kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha jambo ambalo liliwalazimu
kuendesha gari taratibu sana. Walikuwa wanaelekea hoteli walikokuwa wanakaa kwa
kipindi chote cha utalii wao, njiani walimuona mtoto kalala nje ya nyumba na
mvua ilikuwa ikinyesha sana. Walishangaa sana hivyo walichukua mwamvuli na
kuisogelea ile nyumba. Walipofika pale waligundua kuwa mtoto kazimia,
lakini Exhao alijikuta kampenda yule mtoto hivyo akamwambia mumewe kuwa; yaweza
kuwa bahati yao kupata mtoto kwa njia ile, alisema vile baada ya
kuhisi yule mtoto atakuwa yatima, na pale atakuwa hakuwa na pakulala wakati
mvua ilipoanza ndiyo maana kazimia.
waliamua kumchukua yule mtoto, wakati
wanambeba, viatu vilimtoka yule mtoto, lakini hawakujali. Walipoingia na
yule mtoto kwenye gari, Exhao alitoka na maua na akaenda
kuyaweka pale mwenye viatu akiwa na maana kuwa, anafuraha na mahali pale
maana ndipo pamemsaidia yeye kupata mtoto.
Waliondoka na Elvine mpaka kwenye hoteli
waliyokuwa wamefikia. Kwakuwa walikuwa wanaondoka siku inayofuata
waliona inaweza kuwapa shida kuondoka na yule mtoto hivyo asubuhi walimchoma
sindano ya 'nusu kaputi' na wakamuweka kwenye boksi na kuondoka naye hadi China
ambako walimpeleka kwenye hospitali yao ambayo wao ndio walikuwa wamiliki wa
Hospitali hiyo. Na baada ya Elvine kutibiwa na kupona walijitahidi kutafuta
uhalalisho wa mtoto yule kuishi pale nchini na wakafanikiwa. Tatizo lilikuwa ni
moja tu, Elvine hakuwa yatima kama walivyojua na baada ya kujua hili Mr. Ezhu
yang aliamua kumfuta kumbukumbu Elvine ili aweze kummiliki kama mwanaye
halisi.
Exhao hakutaka wamfute kumbukumbu maana
alimuwaza mama wa mtoto Elvine atakavyochanganyikiwa. Alitamani amrudishe
lakini yeye pia alishampenda Elvine.
Baada ya Exhao kuwaza sana akaona hana
jinsi zaidi ya kukubaliana na kilichotokea.
Elvine alipelekwa hospitali baada ya
kuchomwa ile sindano lakini walishangaa kuona Elvine haamki. Wote hawakujua
sababu ya Elvine kutokuamka maana kila kitu
kilifanyika vizuri kabisa. Siku tatu zilipita lakini Elvine bado hakuamka, hili
liliwachanganya sana madaktari pamoja na familia ya Mr. Ezhu yang
Usiku wakati Exhao kalala aliota ndoto kuwa
Elvine anamuita, tena kwa jina lake la Exhao Ebrow. Aliposhituka
kutoka usingizini ilikuwa ni saa 6:00 usiku. Exhao aliamka
usiku ule pasipo kuaga aliondoka na kuelekea hospitali.
Alipofika
hospitali aliingia moja kwa moja mpaka kwenye chumba cha Elvine: kwakuwa
haikuwa shida kuingia maana hospitali ile yeye na mumewe ndiyo walikuwa
wamiliki, yaani ilikuwa hospitali yao binafsi.
Alipofika
chumbani alimkuta Elvine bado kalala hajitambui kabisa. Alianza kusogea pale
kitandani kwa Elvine huku akimsemesha Elvine ambaye alijua kabisa kuwa Elvine
hasikii.
"Am sorry
Elvine my son, it's our fault"(samahani Elvine, ni makosa yetu). Alipofika
karibu na kitanda alicholalia Elvine ghafla taa ilizima. Yule mama alijikuta
kapata woga sana maana kulikuwa giza ambalo lilimfanya asione hata hatua moja
mbele. Aliingiza mkono kwa pupa kwenye mkoba wake ili atoe simu kwaajili ya
kuwasha tochi, lakini kabla hajatoa simu alishangaa kuona mwanga ndani ya
chumba kile. Alitazama taa juu lakini ilikuwa haiwaki.
Aligeuka na
kumtazama Elvine. Alishituka na akaogopa sana kwa kile alichokiona, maana
Elvine alikuwa anawaka mwili mzima kana kwamba yeye ndiyo taa.
Yule mama
alirudi nyuma na kwa woga alipiga kelele lakini kulikuwa kimya sana. Wakati
kasimama hajui afanyenini alibaki kajishika mdomo kama anayejizuia kuongea zaidi
au anayeshangaa kupitiliza.
Ghafla Elvine
aliamka pale kitandani na akawa anatabasamu. Alipomtazama Exhao aliona kama
tumboni kwa Exhao kuna mtoto mdogo wa kama miezi mitatu hivi toka kuzaliwa, akatabasamu
na yule mtoto akatabasamu pia, Elvine akaanza kusogea pale Exhao aliposimama,
na wakati huo Exhao naye akawa anarudi nyuma.
Wakati Elvine
anamsogelea Exhao alishangaa kuona yule mtoto aliyekuwa tumboni kwa Exhao
amekabwa na mnyororo wa moto na palepele yule mtoto alikufa. Elvine alianza
kulia kwa uchungu sana lakini akasikia sauti ikimwambia "why can't you
save that woman? Save her with her child" (kwanini huwezi kumsaidia huyo mwanamke,
msaidie yeye na binti yake).
Elvine alifuta
machozi na akasogea mpaka alipokuwepo Exhao, kisha akamshika yule mama tumbo na
akasema "Elvila you can't die" (Elvila huwezi kufa) mara akaona yule
mtoto kaamka na ile minyororo ikateketea. Elvine alitabasamu na akasema huyu ni
mdogo wangu mimi kwahiyo apewe jina la rafiki yangu Elvila. Baada ya kusema
vile mlango ulifunguliwa na madaktari ambao kumbe waliisikia ile sauti ya Exhao
ya kupiga kelele. Walipoingia tu, taa iliwaka. Ghafla Elvine alianguka pale
chini na kupoteza fahamu tena.
Exhao hakuwa
anaona kama kuna mtoto tumboni mwake wala hakujua chochote kilichoendelea pale
ndani zaidi alichojua yeye ni kwamba Elvine aliamka na kushika tumbo lake.
Kwa yale aliyoyaona
mule chumbani Exhao hakuwa na hamu ya kubaki mule ndani, mlango ulipofunguliwa
tu, aliona kama amefunguliwa kutoka kwenye gereza lenye wadudu na wanyama wa
kila namna duniani, maana alikimbia kama kichaa. Kila mtu alimshangaa.
Alikimbia mpaka nyumbani, na alisahau kabisa kuwa alikuja na gari pale
hospitali, hivyo 'miguu niokoe' hadi alifika nyumbani. Alipofika nyumbani
alimkuta mume wake kalala. Kwa woga aliokuwa nao alijirusha kitandani kama
muogeleaji aliye kwenye mashindano ya kupiga mbizi. Mr. Ezhu yang alishituka na
akamuuliza nini kilichotokea, lakini hakuwa na uwezo hata wa kuongea na zaidi
alitaja tu jina la Elvine.
Mr. Ezhu yang alishangaa sana lakini alimtuliza mkewe mpaka Exhao
alipolala na yeye ndipo akalala.
Asubuhi walipewa taarifa kuwa Elvine kaamka. Exhao aliposikia zile
habari alichanganyikiwa maana tayari alianza kumuogopa Elvine kwasababu alikuwa
anajiuliza maswali mengi sana kuhusu yule mtoto Elvine na akaanza kujuta
kwanini alichukua mtoto wa watu asiyemjua. Lakini hakumwambia mtu kilichotokea
na hata alipotaka kusema alijiona mzito sana kuzungumza, kwahiyo ilibaki kuwa
siri yake.
Jioni Elvine alirudi nyumbani, na vipimo vilionesha kuwa ni kweli Elvine
hakumbuki chochote.
Elvine alikaa nyumbani wiki moja na alishangaa sana kuona namna Exhao
anavyomuogopa na kumnyenyekea, kiukweli hata yeye hakuwa anakumbuka chochote
kilichotokea ule usiku wa maajabu kwa Exhao. Elvine anianza kufundishwa kila
kitu na akaambiwa kuwa yeye ni mtoto wa palepela China ila ni mwafrika kwakuwa
wazazi wake walikuwa waafrika japo walikufa yeye akiwa mdogo.
Elvine alianza shule, lakini
tofauti kabisa na kwao, huku hakuweza tena kufundishwa mambo ya Mungu. Alipoanza
shule wale rafiki zake wa mwanzo walishangaa sana kuona Elvine hawakumbuki,
kwahiyo waliamua kujitambulisha upya kwa Elvine, nao walikuwa ni Elimina, Ester
na Emmanuel, wote hawa walikuwa watanzania. Baada ya Elvine kupoteza kumbukumbu
hakuweza kupata taarifa zozote kutoka kwa rafiki zake maana hakuwahi kuwaambia
historia yake kamili.
Kila likizo rafiki zake walikuwa wakirudi Tanzania kwenye familia zao
lakini Elvine hakuwa anajua kama kwao ni Tanzania, japo rafiki zake walimuambia,
lakini hakuwa anaamini maana hata kiswahili kilianza kumpotea kichwani, jambo
ambalo liliwafanya rafiki zake waanze kumfundisha tena kiswahili.
Baada ya miezi mitatu kupita Exhao aliaanza kujihisi tofauti sana. Na
baada ya kupima aligundua kuwa anaujauzito wa miezi mitatu. Hakuamini kabisa
maana alishawahi kuambiwa kuwa hatopata mtoto kabisa. Exhao alifurahi sana
lakini hata mume wake alifurahi zaidi. Baada ya Exhao kujua kuwa kabeba mtoto
wa kike tumboni mwake ndipo alipokumbuka ile siku ambayo Elvine alipokuwa akiwaka
moto pale hospitali, na akakumbuka maneno ya Elvine kuwa "huyu ni mdogo
wangu Elvila" kwahiyo mtoto alipewa jina la Elvila kama Elvine alivyosema
ile siku, na baada ya hayo Exhao ndipo alipomsimulia Mr. Ezhu yang kilichotokea
kule hospitali ule usiku. Wote walianza kumpenda sana Elvine na wakaona kama ni
mtoto wa baraka na miuzija kwenye familia yao.
Elvine alisoma hadi akafika chuo kikuu na akawa hajui kabisa asili yake
kuwa ni Tanzania. Rafiki zake walikuwa wakimwambia lakini hakuamini kabisa na
yeye alikuwa akiwapenda sana wazazi wake na mdogo wake Elvila pasipo kujua
ukweli.
Akiwa chuo yeye alikuwa hasali kabisa maana hata familia yake hawakuwa
wanasali. Lakini Elimina na Ester walikuwa wanamwambia sana habari za yesu
lakini hakuwa anaelewa. Emmanuel na Elvine walipofika chuo wakawa wasumbufu
sana, maana walipenda kwenda 'clab' na Elvine akaanza kunywa pombe.
Elimina na Ester waliwaonya sana rafiki zao lakini hawakusikia. Taarifa
za kunywa pombe kwa Elvine ziliwachukiza hata wazazi wake maana walikuwa
wanamuona kama mtoto mtakatifu baada ya wao kupata mtoto. Lakini hali haikuwa
kama walivyodhani, maana Elvine alikuwa ni shida pale nyumbani. Ilifika wakati
anaweza akakaa nje wiki bila kurudi nyumbani.
Hali ilizidi kuwa mbaya na baadaye akaanza kuvuta bangi, makundi ya chuo
yaliwaharibu kabisa, lakini "Mungu anawajua walio wake!". Siku moja
akiwa amelala baa baada ya kulewa sana aliota ndoto.
"Moto mkubwa ulikua unawaka katika maji, Elvine alizidi
kusogea pale huku akistaajabu sana, na aliogopa sana "haaa! hivi inawezekanaje
moto
uwake ndani ya maji? au ndio ile muvi ya jana inajirudia ila huu nii
muendelezo wake? Akiwa anashangaa alimuona Eliana, Ester na Elvila pembeni na ilikuwa
ni kanisani. Elvila akamwambia, 'Elvine wewe si mtumishi wa mungu eeh?'"(zilikuwa
ni kumbukumbu za utotoni)
Elvine alishituka sana na akajikuta baa,
aligundua kuwa kaibiwa hela zote alizokuja nazo siku hiyo baa. Moyo ulianza
kuuma na akawa anasikia sauti kichwani mwake ya mtu ambaye alikuwa akipiga
kelele akimwambia " wewe ni naniiiii!? Wewe ni naniiiii? Wewe sio
Elvine" alianza kuona kizunguzungu, alilia sana pasipo kupata msaada na
ndipo akamkumbuka Editrin mama yake. Akasema "mama yangu ni Editrin!!!...
Sehemu ya tano itaendelea jumatano >>>>>. Usikose kufuatilia.
Bonyeza hapa kupata mwendelezo wake
Hadithi hii imendaliwa na kuandikwa na JACQUELINE JOHN.
Mwimbaji
na mtunzi wa nyimbo, mashairi, Hadithi (simulizi) na ngonjera.
Mawasiliano:
Whatsapno. >>>>>
+255789523850. Normal >>>>>+255747313148.
Na,
Imehaririwa na MIGONGO ELIAS. Mhariri.
Mawasiliano:
Whatsapno. >>>>>
+255767653697. Normal >>>>>+255783327456.
GeT tO tHe NeXt LeVeL!
Kama umejifunza kitu shiriki nasi katika
comment hapo chini, ili kujifunza na kuboresha zaidi.
Sort by: Date Rating Last Activity
Comments by IntenseDebate
Posting anonymously.
Jacob · 94 weeks ago
Elias · 94 weeks ago
Chyo · 94 weeks ago
Migongo · 94 weeks ago