HATIMA YA KIMUNGU SEHEMU YA 31

Image
  HATIMA YA KIMUNGU SEHEMU YA 31 Ilipoishia………. Elvine alipoteza amani kuliko hata mkewe maana kila alipomtazama mkewe basi moyo wake ni kama ulikuwa unachomwa na mwiba uliojishikiza huko kwenye mishipa ya moyo. Nafsi yake ilitaabika na ndipo alipoamua kutafuta muda mzuri, baada ya chakula cha jioni, azungumze na mkewe, maana ule ukimya wa siku mbili ulikuwa adhabu kubwa sana kwake. Kusoma sehemu ya 30 bonyeza hapa Sasa inaendelea………. Elimina mamy naomba kujua kwanini hutaki kuniuliza kuhusu sababu ya haya yote? Maana najua unajua kuwa kuna mahali mimi nilikosea, sasa unapokaa kimya hivyo… kiukweli unazidi kunichanganya maana ni kama hutaki kujua, sasa unadhani mimi roho yangu itatulia kweli?. Hata kama ungekuwa wewe lazima usingepata amani, ungekuwa hata unawaza hivi nakuwaziaje, nakuonaje na ninajisikiaje ninapokuona, sasa kwanini wewe umekaa kimya, sema neno tafadhali? (Elvine alikuwa akiongea bila kumtazama mkewe usoni maana moyo wake haukuwa katika hali ya utulivu). Pamoja na ...

SIMULIZI YA KUFURAHISHA, “KUHUSU HATIMA YA KIMUNGU”. SEHEMU YA TANO.

 

SIMULIZI YA KUFURAHISHA, “KUHUSU HATIMA YA KIMUNGU”.

SEHEMU YA TANO. 

 Ilipoishia..........

 Elvine alishituka sana na akajikuta baa, aligundua kuwa kaibiwa hela zote alizokuja nazo siku hiyo baa. Moyo ulianza kuuma na akawa anasikia sauti kichwani mwake ya mtu ambaye alikuwa akipiga kelele akimwambia " wewe ni naniiiii!? Wewe ni naniiiii? Wewe sio Elvine" alianza kuona kizunguzungu, alilia sana pasipo kupata msaada na ndipo akamkumbuka Editrin mama yake. Akasema "mama yangu ni Editrin!!!...

Kama hujasoma sehemu iliyopita bonyeza hapa

 Sasa inaendelea...

 Elvine alirudisha kumbukumbu ghafla na akakumbuka kila kitu kuhusu familia yake. Alilia sana kwa majuto ya kumtelekeza mama yake Editrin. Hakujua kwanini Mr. Ezhu yang aliamua kumdanganya na hakujua kwanini alisahau kila kitu kwa kipindi kifupi hivyo. Elvine alikuwa na miaka 23 sasa, na aliondoka kwao akiwa na miaka 15.

     Kwa hasira aliyokuwa nayo alipanga kurudi nyumbani na kuleta fujo kwa Mr. Ezhu yang lakini akakumbuka asili yake ya kweli kuwa yeye ni mtoto wa kikristo na hakufundishwa tabia mbaya wala ugomvi na mama yake Editrin.

    Aliwaza cha kufanya akakosa majibu. Mwisho aliamua kurudi nyumbani ili akapate taarifa kamili kutoka kwa walezi wake wale.

      Akiwa njiani kurudi nyumbani alikutana na Elimina.

   "Elvine!"

   "Yes"

   "Are you ok?"(upo sawa)

   "I don't know Elimina, I don't know."(sijui Elimina, sijui). Elvine alipomtazama Elimina alishindwa kujizuia kabisa na machozi yalianza kumdondoka. Elimina alishangaa maana hakuwahi kumwona Elvine kwenye hali ile toka amfahamu. Mwisho Elimina alimshika mkono na kutafuta hotel nzuri ili waweze kuzungumza. Elvine alimsimulia historia yake kwa urefu sana hasa maisha yake alipokuwa mdogo, namna alivyojikuta China, na namna alivyojikuta kapoteza kumbukumbu.

   Elimina alionyesha kuguswa sana na stori ya Elvine na yeye akawa anatamani sana kujua sababu ya Elvine kuletwa China na kuhusu mama yake Editrin. Kama ilivyo kwa Elvine na ndivyo ilivyokuwa kwa Elimina maana Elimina alionekana kuwa na tabia nzuri sana na moyo wa huruma sana, hivyo wakakubaliana kuwa watakwenda wote kufuatilia kuhusu sababu ya Elvine kutenganishwa na mama yake maana walihisi itakuwepo sababu.

   Elimina naye alimueleza Elvine kuwa yeye ni mtoto wa mchungaji anayeitwa 'Moses'. Na hapo ndipo Elvine alipomtambua Elimina kuwa ni yule mtoto aliyewahi kumuona akiwa mdogo, Elvine Alishangaa sana na mwisho akajikuta kasema

 "kumbe ni wewe?"

 "Mimi nini?"

 Baba yako niii... Elvine alisita kidogo na akajikuta katabasamu, halafu hakuendelea kuzungumza. Elimina hakujua kama walishawahi onana wakiwa Tanzania.

   Wakati huo Elvine alikuwa kasha pata wazo na namna anavyoweza kumtumia Elimina kufika kwao, kwahiyo aliamua kukaa kimya kwanza.

  *     *     *     *    *     *      *      *      *    

Huku Tanzania baada ya Elvine kupotea Editrin aliamua kukubali kuambatana na mama yake, hivyo alirejea tena Dar es salaam kwa baba yake na mama yake. Alipofika nyumbani baba yake alionyesha kufurahia sana binti yake kurudi nyumbani.

     Mr. Edward hakumsumbua tena binti yake na aliomba msamaha lakini hakukili kosa la kumuua Edwin. Editrin alishindwa kumsamehe baba yake kabisa kwasababu ya Edwin, na alikuwa akimchukia sana baba yake maana alimuona kama shetani kwake maana kwake yeye aliona baba yake ndiye chanzo cha kusambalatika kwa familia yake.

     Editrin akiwa kwa baba yake alishangaa sana namna baba yake alivyobadilika na kuwa mpole sana. Mr. Edward alibadilika na akawa ni mtu mwenye mawazo sana na mara nyingi alikuwa akichelewa nyumbani jambo ambalo lilimfanya mama yake Editrin kuwa na mgogoro na mumewe kila siku kwa kuhisi mumewe kaanza uhuni.

     Mr. Edward alizidi kuonekana kama mtu asiye na amani kabisa, na mwisho alianza ulevi na uchelewaji ukazidi.

    Siku moja Editrin aliamua kumfuatilia baba yake ili ajue baba yake huwa anakwenda wapi baada ya kutoka kazini maana alimhurumia sana mama yake kwa namna alivyokuwa hana amani, lakini pia alifanya hivyo kwakuwa mama yake ndiye aliyemuomba afanye kazi hiyo.

       Alifika nje ya ofisi ya baba yake na gari lake ambalo alipewa baada tu ya kurudi kutoka Iringa. Hakushuka haraka kutoka garini bali alisubiri baba yake amalize kazi, na alijua kuwa akiwa pale ataweza kuona kila mtu atakaye kuja pale ofisini siku hiyo.

   Alikaa pale nje hadi jioni;  alihisi njaa sana. Hivyo akashuka kwenye gari na kuenda kununua chakula kwenye hoteli iliyokuwepo jirani na ofisi ya baba yake. Alinunua chakula na kurudi tena kwenye gari lake.

   Alikaa garini kwa mda mrefu hadi giza likaingia lakini hakuona baba yake akitoka ofisini, alipotazama kwa makini aligundua kuwa kuna gari lipo pembeni ya gari lake ambalo hakuliacha wakati anaenda kununua chakula. Hivyo aligundua kuwa kuna mtu kaingia ndani ya ofisi.

     Alikaa hadi saa 2:50 usiku na akaona kachoka kusubiri, hivyo aliwasha gari na kuondoka. Alipofika nyumbani alimwambia mama yake kuwa baba yake hajatembelewa na mtu yeyote leo na wala hajatoka ofisini. Kiukweli alidanganya lakini hakuwa na uthibitisho ambao ungemfanya aseme ni nani aliyekuja ofisini siku hiyo.

   Ulipofika Usiku muda kama wa saa 5:20 hivi alisikia kelele za baba yake kutoka sebuleni, kelele zile ziliashiria kabisa kuwa baba yake kalewa. Na alipiga kelele za kumuita yeye. Zile kelele ziliwashitua hata wafanyakazi wa mule ndani hivyo wote walikuja sebuleni kuona ni nini kinachoendelea. Editrin na mama yake pia waliwasili sebuleni.

    Mr. Edward baada ya kumuona Editrin amekuja sebuleni alimfuata na kumpiga vibao viwili vya mfululizo ambavyo vilikuwa ni vizito mno kwa Editrin. Jambo lile liliwashitua watu wote pale ndani. Mr. Edward akaanza kufoka kilevi huku akitoa akonyesha kuongea kwa uchungu kama anayetaka kulia.

  " Hivi we mtoto mbona unabalaa? Mimi mbona nimekuacha na maisha yako, lakini wewe hutaki nikuache?. Haya niambie sasa, ofisini kwangu ulikuja saa ngapi? Na nani alikuita kule? Mimi ningekua nataka uje kazini si ningekuita?. Wewe mtoto huna akili. Na mimi sikutaki tena."

    Editrin alilia sana na kwauchungu na yeye akajibu kwa hasira sana

    "Kwani nani kasema mimi wewe ni baba yangu, kwakweli nazidi kujua namna ambavyo unanichukia. Sawa nitaondoka na sitaki mnitafute, niacheni na maisha yangu basi. Yaani umeharibu familia yangu bado huridhiki tu? Au unataka nife na mimi?" Editrin aliongea kwa hasira sana na baada ya kuongea vile aliondoka mpaka  chumbani kwake ambako alijifungia na kulia sana. Haikuwa hivyo kwake tu hata Mr. Edward aliingia chumbani na akawa analia sana huku akisema kwanini imekuwa hivi.

    Mkewe hakujua ni nani amfariji kati ha binti yake au mume wake Edward. Lakini hakuwa anajua kwanini Edward analia kiasi kile. Edward alionekana ni kama anayejutia jambo, lakini hakuweza tu kueleza. Eliana alihisi labda pombe ndizo zilizomchanganya mumewe.

     Asubuhi Mr. Edward aliondoka mapema sana na kwenda kazini. Editrin alipoamka alikuwa kashajiandaa kuondoka pale nyumbani pasipo kujua hata anakwenda wapi, lakini mama yake aliomba msamaha mwa niaba ya mume wake na akamsihi binti yake asiondoke.

    Usiku ulipofika Editrin alikuwa nje ameketi kwenye amua anawaza kuhusu maisha yake. Akiwa pale aliona gari la baba yake linaingia, wakati anaendelea kuwaza alimwona baba yake akipokea simu na alionekana kugombana na mtu.

    "Hivi wewe shida yako ni nini?, Wewe umeshaoa? ...... Huwezi kusema makubaliano hayajavunjika wakati wewe tayari una familia. .... Nimesema hapana Editrin siwezi kumtumia kama bidhaa tena. ... . Sawa lakini ..... Haiwezekani unifanyie hivyo .... Hivi lazima awe Editrin tu?. Hapana... Hapana.... Sina maana hiyo". Simu ikakatwa, Mr Edward alichukia sana na akaingia ndani kwa hasira sana na leo hakuwa kalewa Kama siku nyingine na pia aliwahi kurudi nyumbani.

       Yale mazungumzo yalimfanya Editrin apate maswali mengi sana, na ndipo akaanza kuhisi kuwa kuna jambo nyuma ya pazia ambalo yeye anaweza kuwa halijui. 

     Alisubiri baba yake aingie ndani na yeye ndipo alipoingia ndani na kwenda kulala. Usiku aliwaza sana. Akiwa katika mawazo mengi sana alipitiwa na usingizini na ndipo alipoota ndoto ambayo ilimfanya aone Edwin hakuuwawa na baba yake bali ni mtu mwingine ambaye ndotoni hakumtambua kabisa lakini sio baba yake. Alishituka sana lakini akajisemea mwenyewe kuwa ile ni ndoto tu.

     Asubuhi alipoamka alikosa amani kabisa na kile alichokiota kikawa kinazidi kuitesa akili yake. Alimsimulia mama yake ambaye alimwambia aendelee kuomba Mungu wake tu maana hata haelewi chochote.

     Editrin aliamua kumfuatilia baba yake tena na wakati huu hakuishia nje ya ofisi bali aliingia hadi ndani ya ofisi ili apate ukweli kamili wa yeye kuzuiliwa kwenda ofisini kwa baba yake. Ofisini alimkuta baba yake anaendelea na kazi zake za kila siku.

     Kitendo cha Edward kumwona binti yake ofisini kilimshitua sana, jambo ambalo hata Editrin aliligundua, yule baba alisogea kwa Editrin na akamwambia hatakiwi kuwepo pale muda ule labda wakati mwingine. Editrin hakuwa tayari kuondoka. Mr Edward alijishusha na akaanza kama kumbembeleza kwa upole Editrin aondoke. Editrin alishangaa sana, alipomuuliza sababu alimwambia atakuja kumwambia pindi atakaporudi nyumbani. Wakati wanaendelea kubishana, ghafla aliingia Esau ambaye naye alionyesha kutotarajia kumwona Editrin pale.

     "Haa Editrin? Ni wewe kweli? Oooh dear ni muda sana hatujaonana, hivi umerudi lini? Maana kuna siku nilikuona kwa mbali lakini sikuwa na uhakika kuwa ni wewe" baada ya kusema vile Editrin aligundua sababu ya baba yake kurudi ule usiku akiwa na hasira,

   "Inamaana lile gari lilikuwa la Esau na Esau ndiye aliyeniona mimi na kwenda kumwambia baba japo mimi sikumuona. Sasa kwanini Esau anaonekana kama anajambo la siri na baba yangu?" Editrin alijiuliza kimoyo moyo.

     Mr. Edward alimwambia Editrin akakae nje mara moja. Editrin alikubali kuwapisha kidogo. Lakini hakwenda mbali bali alijibanza ukutani na kuanza kuwasikiliza.

     "Sikiliza Esau Mimi siwezi kuruhusu umuoe Editrin, maana nimegundua wote ni ujinga, halafu mbona baba yako katulia tu hana shida, tatizo lako ni nini wewe? Halafu isitoshe wewe tayari unamke."

     "Ooh, hilo lisikutishe Mr. Edward. Mimi bado nampenda binti yako sana tu, na hata sijali kuhusu hilo. Nachotaka ni kuwa lazima wewe unipe Editrin"

     "Kwani kunaulazima gani wa wewe kufanya hivyo?"

    "Sikiliza mzee, hii pia ni biashara, na sitaki kubishana maana malikia wangu mtarajiwa asije akasikia hapo nje halafu ikawa balaa. Kama nilivyokwambia mwanzo wewe fanya maamuzi kati ya mimi kuivuruga hii kampuni yako ya "A quality" au kunipa binti yako. Na Kama unavyojua mimi nikisema nimeshasema. Uamuzi ni wako mzee"

      Editrin alisikia yale yote na ndipo alipogundua kuwa baba yake hakuwa anamuozesha yeye kwakupenda lakini alikuwa akilazimishwa na Esau na familia yake kwasababu za kibiashara maana, Esau na familia yao walikuwa matajiri kuliko wao. Sasa Editrin akawa na swali moja kichwani "kwanini baba yake ahusike kwenye kifo cha mumewe? Na kama hahusiki basi kuna kitu anajua, sasa kwanini akae kimya?"

     Editrin aliamua kuondoka kwenda kanisani; maana ilikuwa jumatano siku ya ibada ya jioni.

        Alipofika kanisani ibada ilikua haipandi kabisa maana alikuwa na vitu vingi sana kichwani. Siku hiyo alimuona mtoto mdogo pale kanisani ambaye umri wake ulifafa sana na Elvine kabla hajapotea. Editrin alijikuta akimkumbuka sana kijana wake, na hapo ndipo aliposhindwa kujizuia baada ya kuikumbuka familia yake na kuanza kulia, moyoni mwake alikua na neno moja tu "walionidhurumu familia yangu lazima walipe hata Kama ni baba yangu. Sitomsamehe".

   Kanisani somo la msamaha lilihubiriwa sana, lakini hayakuwahi kupata nafasi kwake. Somo la msamaha lilipohubiriwa alikuwa akilia sana jambo ambalo wengine wangeweza kuhisi labda kashukiwa na roho wa Bwana au amesamehe mtu aliyemuumiza sana. Lakini ukweli ni kuwa alikuwa akilia kuomba msamaha kwa Mungu kwa kusema Mungu amsamehe tu lakini hawezi kusamehe mpaka adui zake walipe ubaya wao. Neno la muachie Mungu lilimkera japo alikuwa wa kwanza kusema Amina! Lakini haikuwa ya kweli maana moyoni mwake ulijaa uchungu usiopimika.

Akiwa kanisani baada ya ibada kuisha, aliamua kufanya maamuzi magumu sana ili tu aweze kumpata adui wa familia yake, hivyo alisogea mbele ya madhabahu na akasema maneno machache tu lakini yalibeba uchungu na kiapo hatari sana.

"Mungu nisamehe kwa huu uamuzi lakini no matter what, lazima nimjue aliye na mtoto wangu na aliyemuua mume wangu. Mungu ni rehemu Kwahaya maamuzi lakini naomba baraka zako maana siwezi kukaa kimya tena. Mpaka hapa nilipofikia basi inatosha Mimi kuumia, maana nahisi hata mtoto wangu hawa watu ndio wanajua aliko. Huu ndiyo mwanzo, nipo tayari kufa, maana Sina cha kupoteza.  nisamehe sana ila niruhusu tu mimi nifanye hivi please..."

Sehemu ya tano itaendelea ijumaa >>>>>. Usikose kufuatilia.

Bonyeza hapa kupata mwedelezo wake

Hadithi hii imendaliwa na kuandikwa na JACQUELINE JOHN.

Mwimbaji na mtunzi wa nyimbo, mashairi, Hadithi (simulizi) na ngonjera.

 Mawasiliano:

Whatsapno. >>>>> +255789523850. Normal >>>>>+255747313148.

                            Na, 

Imehaririwa na MIGONGO ELIAS. Mhariri.

Mawasiliano:

Whatsapno. >>>>> +255767653697. Normal >>>>>+255783327456.

                                            GeT tO tHe NeXt LeVeL!

Kama umejifunza kitu shiriki nasi katika comment hapo chini, ili kujifunza na kuboresha zaidi.

 

    

 

 

Popular posts from this blog

MAAJABU YA AKIBA

UCHAMBUZI WA KINA HATIMA YA KIMUNGU SEHEMU YA 29

UCHAMBUZI WA KINA HATIMA YA KIMUNGU SEHEMU YA 27.