HATIMA YA KIMUNGU SEHEMU YA 31
MAISHA YAKO NA WATU.
Pamoja na kuwepo kwa maelfu na mamilioni ya viumbe hai katika dunia hii. Binadamu bado ni kiumbe wa muhimu sana na mwenye upekee wa hali ya juu, ukilinganisha na viumbe wengine. Hii pengine ni kutokana na akili, utashi, hekima, na mamlaka ambayo ameumbiwa na kupewa na Mungu. Kwa ufupi dunia inang’ara, kuvutia, kupendeza, na kuwa kama paradiso kutokana na kuwepo kwa binadamu. Ajabu ni kwamba wakati mwingine, dunia inachafuka, kuharibika na kuwa kama jehenamu kutokana na kuwepo hao hao binadamu, pengine labda kwakuwa hakuna kizuri kisicho kuwa na hasara eeh!
Lakini,
tuseme tu ukweli binadamu wamekuwa ni sehemu muhimu sana katika kurahisisha na kufanikisha mambo hapa duniani. wapo watu tunao wafahamu na wengine hatuwafahamu kabisa
lakini wamerahisisha sana maisha tuwapo hapa duniani, mara tu baada ya kukutana
nao.
Hivi ulishawahi kujiulizakwamba, maisha bila watu
yangekuwaje? Je mpaka hapo ulipo ungefikaje? Kuna namna maisha yangekuwa
songombingo, hii ni kusema maisha bila watu asee tungepata tabu sana. Maana yake,
hata barabara zisingekuwepo, hospitali zisingekuwepo, shule zisingekuwepo,
maduka yasingekuwepo, nguo zisingekuwepo na mambo mengine kede kede,labda tu Mungu angevishusha moja kwa moja. Mimi sijui
ingekuwaje lakini kama unafikiri kama mimi, nadhani umeanza kupata picha vile
maisha bila watu yangekuwa.
Ni muhimu kufahamu kwamba, kila mtu ameumbwa kwa kusudi na kazi maalumu hapa duniani. changamoto ya watu wengi ipo kwenye kuligundua na kuliishi kusudi hilo. Kuwepo kwa kazi, vipaji, kusudi, na malengo tofauti tofauti kwa watu ambayo kila mtu amepewa ili kuwahudumia watu wengine awapo hapa duniani. kitu hiki pekee ndiyo kimekuja kurahisisha maisha tuwapo ulimwenguni. Kama mtu akiamua kuligundua na kuliishi kusudi lake na kuwasidia wengine kutimiza ndoto zao, watu wa namna hii, ndiyo huifanya dunia kuwa kama paradiso ndogo hapa duniani.
Na kinyume chake ndiyo
kweli, kwamba watu watakao amua kuishi nje ya kusudi lao, hawa ndio huishi
maisha ya balaa, hasara na majuto sana hapo baadae. Na pengine hawa ndiyo huifanya dunia ifanane
na jehanamu kwa matendo yao.
Mtu mmoja amewahi kusikika akisema “watu ni maktaba inayotembea”. Akimaanisha kuwa watu wanayo mengi sana ya kukufundisha na kukusaidia kufikia ndoto yako kwa urahisi zaidi. Ukweli ni kwamba, kwa kuwa kuna kusudi ambalo Mungu ameweka ndani yako ili ulitimize na uwasaidie watu wengine, hata wewe kuna watu Mungu atakuandalia na kukuinulia ili upate wepesi na njia ya kuziendea ndoto zako. Ndiyo maana, katika kila sehemu au hatua ya maisha yako ukifika utakutana na watu fulani, yaweza kuwa unawafahamu au huwafahamu kabisa. Lakini, watafanyika kuwa baraka kwako hadi mwenyewe utashangaa na watu hawa wanaweza kutokea kwa muda mfupi tu au kwa muda mrefu kwenye maisha yako.
Sikiliza ndugu, asilimia kubwa, Mungu akitaka kukubariki au kukujibu
mahitaji ya moyo wako, hutumia watu. Hapa ndipo utakuja kushangaa kwamba
kuna namna maisha yako yalianza kubadilika baada ya kukutana na watu fulani
kwenye sehemu ya maisha yako. Watu hawa yawezakuwa
ni marafiki, majirani, watu baki, mwenza au ndugu. Na wanaweza kuwa wa baraka
sana kwako kama utafanikiwa kukutana nao sehemu na muda sahihi. Tambua kwamba, watu
hawa wanahitaji kutambuliwa na huwa wanakuja kwa nyakati tofauti tofauti na
usipo watambua wataondoka na utakuwa umepishana na gari la mshahara.
Lakini kwa upande mwingine wa shilingi kuna watu wao kazi
yao ni kukuchelewesha na kukurudisha nyuma katika kuyafikia mafanikio yako.
Watu wa namna hii watakuvunja moyo, watakukatisha tamaa, watakudharirisha,
watakusema vibaya, na hata kukufanya ujione huna thamani kabisa. Wengine watakufanya
kujiunga na makundi mabaya, vitu kama hivi vitasababisha utoke kwenye reli ya
kuyaendea mafanikio na ndoto zako na hapa ndiyo itakuwa mwanzo wa kuliacha
kusudi la Mungu kwako. Hivyo pamoja na umuhimu mkubwa sana wa watu katika
maisha yetu ni muhimu pia, kufahamu upande mwingine wa
shilingi kwamba watu wale wale wakati mwingine wanaweza kutumiwa vibaya ili
kutuharibia. Na hii ikawa ni mwanzo wa kuharibikiwa kwetu. Lakini, si
watu wote. Kikubwa hapo ni kutambua wakati na majira ya kujiliwa kwako. Kwani,
kuna wakati inatakiwa kuwa sehemu fulani na kukutana na watu fulani ili
wakusukume kwenda viwango vingine, na kazi yao ikiisha inawapasa kuondoka ili
kuwapisha watu wengine watakao kupeleka mbali zaidi.
Watu, watu, watu! Watu ni hazina, watu ni mtaji, watu ni maktaba inayotembea watu ni fursa watu ni daraja nasema wazingatie watu.
Nakumbuka Mahatma Ghand aliwahi kusema nikiwatazama watu naona fursa na alipoulizwa kivipi ukiwatazama watu unaona fursa akasema, nikiona nyuso zao naona kesi zao na hapo ndipo natafuta suluhisho lao. Ingekuwa ni kingereza ningesema “wheni I see people I see opportunities. When I see their faces I see their cases that makes me to come out with their solutions”.
Je wewe ukiwatazama watu unawaona kama nini? Je huwa
unajifunza nini kutoka kwa watu? Je watu wananufaika vipi kutokana na kuwepo
kwako? Ndugu yangu kuna namna unatakiwa kubadili mtazamo wako juu ya watu unao
kutana nao. Tambua kuwa watu wana majibu yako, watu wanapesa zako, watu
wanamtaji wako, Tambua kuwa watu wana biashara yako yako, watu wana mashamba yako na sema watu ni
hazina watumie wakufaidishe. Ishi vi zuri na watu, tengeneza mtandao wa watu sahihi kwenye
maisha yako kwani, maisha siyo magumu kiivyo.
Ndugu yangu kwa namna yeyote ile jitahidi kuwasoma na
kuwaelewa watu kwani, kuna wengine wametumwa kukusukuma kwenda mbele zaidi na
wengine wametumwa kukusukuma urudi nyuma zaidi kuwa makini! Na ukiwatambua watu kama hao position yourself utavuka.
Hawa wote ni watu na tunaishi nao, kubwa zaidi tunahitaji jicho la tatu katika
kuwatofautisha watu wa namna hii. Pengine tukijua kuwafahamu watu na nafasi zao
kwetu itakuwa ni fursa kwetu kuwatumia na maisha yetu kuwa rahisi zaidi.
Kubwa kuliko yote watu wengi sana watakuja kwako, wengine
utakutana nao katika harakati zako. Fahamu kuwa WATU HATUFANANI NA
HATUTAFANANA. Kila mtu yupo na upekee wake utafanya makosa makubwa sana
pale utakapo taka kuwa weka watu wote kwenye sehemu na nafasi sawa katika
maisha yako. Badala yake wafahamu watu kwa sifa zao na upekee. Walio nao hii itasaidia sana.
Rafiki, ni matumaini yangu kuwa umejifunza
kitu.
na kama unachangamoto katika hili pengine
namna gani ya kuondokana na adha hii sasa waweza kuwasiliana na mimi moja kwa
moja kupitia mawasiliano hapo chini naamini utasaidika.
GeT tO ThE nExT lEvEl!
Makala hii, imeandaliwa na kuandikwa na MIGONGO
ELIAS Mshauri & Mwalimu Wa Saikolojia, Uchumi na Maisha.
Mwanzilishi na Mwendeshaji wa Mtandao wa addvaluetz. Karibu
sana ujiongezee thamani yako.
Kwa mawasiliano;
Whatsapp & Sim >>+255767653697
/+255783327456
Email>> eliasmigongo120@gmail.com.
Facebook>> MIGONGO ELIAS.
LinkedIn>>Migongoe.
Pinterest>>eliasmigongo.
Kama umejifunza kitu,
niachie maoni yako nitafurahi kujifunza pamoja nawe