MAAJABU YA AKIBA

SIMULIZI YA KUSISIMUA KUHUSU “HATIMA YA KIMUNGU”.
>>SEHEMU
YA TATU.
Editrin
baada ya kutulia alimsimulia kisa kizima mama
yake tangu
alipotoroka kwao, hadi kufikia hapa alipo na namna ambavyo Elvine
alivyopotea. Eliana
alionesha kuumia sana kwani kwa namna nyingine tunaweza kusema yeye ndiye aliyekuwabibi
wa mtoto yule. Wakiwa wanaendelea na mazungumzo yale
Editrin akaanza kukumbuka kisa chote kilichomkuta kwenye maisha yake hata
kupelekea yeye kutoroka kwao Dar es salaam na kuamua kuja kuishi Iringa.......
Sasa inaendelea...,....
Editrin
alizaliwa Katika familia ya kitajiri sana. Baba yake alikuwa akiitwa Mr. Edward
na mama yake aliitwa Eliana. Katika familia yao
walizaliwa watoto wawili tu! ambao ni Editrin na
Edger.
Tangu utoto wao walipendwa sana na wazazi wao wote wawili.
Editrin na kaka yake Edger hawakuwahi kuyajua maisha
ya shida maana baba yako alikuwa na pesa sana. Walikuwa wakiishi jijini Dar
es salaam ambako baba yao alikuwa ni mmiliki wa mabasi ya
"A quality bus".
Kampuni ya Mr. Edward ilipendwa sana na watu
wengi, maana ilisifika kwa kuwa na wahudumu wakarimu na
safari za uhakika.
Editrin baada ya kumaliza sekondari katika
shule ya st. Claudy, alichaguliwa kujiunga na kidato shule ya serikali iliyoitwa
"Kugilwa high school" iliyopo jijini Dodoma. Akiwa shule alikutana
na kijana mmoja alieitwa(aliyeitwa) Edwin ambaye alikuwa ni
kijana wa kipentekoste na alikuwa ni mtu wa imani sana. Kijana
yule alikuwa ni mcheshi sana na alipendwa na kila mtu, alipenda utani lakini
pia, alipenda kuwashuhudia watu wa kila namna na hakusita kuwaambia hata walimu
habari za Yesu kwa namna alivyokuwa anajiamini. Kila
mtu alimpenda. Kwani, hakuwa msema uongo
wala hakupenda ugomvi.
Kwa upande wa Editrin katika
familia yao walikua ni waroma tena wale ambao ibada kwao sio lazima labda kuwe na tukio maalumu kanisani ndipo watakwenda na sio ajabu kabisa
bado watatoka ibada ikiwa haijakwisha. Hata baada ya kufika shule bado hakuwa anapenda ibada japo ibada zilikuwa zikifanyika
kila siku, lakini alikuwa radhi akajifiche chooni hadi muda wa ibada uishe
kisha aende darasani kusoma yaani prepo.
Mkuu wa shule yao alikuwa ni mwanamke aliyeitwa
Emmy . Emmy alikuwa mtu
wa dini sana na
ndiye aliyekuwa
mlezi wa Casfeta pale shuleni, hivyo mama huyo aliweka
sheria kuwa hakuna mtu kuwepo bwenini muda wa vipindi
vya dini,
kila mtu anatakiwa kuwepo kwenye dini yake ifikapo saa 1:00 hadi
saa 2:00 usiku.
Sheria za Emmy zilimkera
sana Editrin hivyo alimwambia baba yake kuwa anahitaji kuhama
shule ile. Wakati akiwa katika mipango hiyo mwalimu wao wa darasa aliyeitwa Emily
alibadilisha ukaaji wa watu katika darasa lake hivyo Editrin akajikuta anakaa
na Edwin sehemu moja.
Kwa ucheshi wa Edwin alimzoea kwa haraka sana
Editrin na wakawa marafika sana. Edwin aligundua kuwa
Editrin alikuwa ni binti asiyependa
ibada hata kidogo, alianza kumshawishi hata kwa zawadi; alimuahidi
kuwa akienda kuwatembelea Casfeta kwa muda wa wiki moja basi
atampa zawadi nzuri sana.
Kwa ule ushawishi wa Edwin,
Editrin alivutiwa kwenda kusali ili apewe tu ile zawadi. Alipokwenda mara ya
kwanza tu, alijikuta anaifurahia ibada ya Wanacasfeta wa
pale shuleni,
maana ilikuwa ni siku ya vishirikishi na kusifu.
Alishangaa
kuona kuwa Edwin alikuwa ni mwimbaji mzuri sana
na ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa Casfeta tawini hapo.
Alizidi kwenda
kila siku, na aliweza
aligundua kitu kingine kuwa licha ya Edwin
kujua kuimba pia alikuwa muhubiri na mshauri mzuri sana kwa watu wengine pale shuleni.
Siku moja katika ibada ya jumapili
usiku ambayo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ili apate zawadi yake, Edwin
alitoa somo ambalo lilimgusa sana Editrin. Somo hilo lilikuwa linahusu kuweka
misingi imara kwa watoto na familia. Na katika maelezo alisema
"kuna watu leo hawampendi Mungu kwa
sababu ya misingi waliyojengewa toka wakiwa wadogo
na familia zao".
Maneno yale yalimgusa sana Editrin na alihisi kama yeye ndiye anayeambiwa
maneno yale. Alilia sana na kwa siku chache zile alizoshiriki ibada alijiona
kama mkosaji sana kwani alijifunza vitu vingi sana hasa
kuhusu Mungu. Editrin aliamua kuokoka na kubadili maisha yake ya mwanzo. Edwin
alifurahi sana kuona kaweza kumfanya rafiki yake aokoke na yeye mwenyewe Edwin
ndiye alimuongoza sara ya toba na kumwombea Editrin.
Tangu siku hiyo Editrin na Edwin
wakawa marafiki wakubwa sana. Edwin kwakuwa alimuahidi rafiki
yake zawadi alikwenda kumnunulia saa ya 5000/= na ulipofika muda
wa prepo baada ya kutoka kwenye kipindi cha dini,
Edwin alimpatia
ile saa Editrin.
"Saa? Mbona inaonekana ya bei ndogo
sana hii!!. Asee!! mimi siwezi kuvaa hii, labda unipe zawadi nyingine"
Editrin alijibu kwa dharau kidogo kuonesha hakuridhika na zawadi aliyopewa. Edwin hakujibu
chochote bali aliichukua ile saa na akairudisha mfukoni mwake kisha akalala
kwenye dawati mpaka prepo ilipoisha na ilipogongwa kengere tu
aliondoka bila hata kuaga.
Ukweli ni kuwa
Edwin hakuwa
mtoto aliyetoka katika familia ya kitajiri kama Editrin. Yeye kwao
kulikuwa ni palepale Dodoma wilaya ya Mpwapwa na kwao walikuwa ni masikini
kabisa. Na zawadi ile ilimgharimu sana maana ilimpasa atoe pesa yake yote ya
matumizi aliyokuwa katumiwa na baba yake
mlezi kwani aliona hakuna shida kama atatoa kwaajili ya rafiki yake huyo maana
chakula shuleni walipewa bure. Aliamua kufanya hivyo kwakuzani kuwa atamfurahisha sana
rafiki yake na pia atamtia moyo kwa uamuzi wake wa kuokoka na kuanza kusali. Lakini daah!! haikuwa kama
alivyotarajia maana, Editrin alizoea kupewa zawadi za gharama sana kwao, kwahiyo
ile zawadi kwake haikumpendeza kabisa. Ni kweli editrin
aliokoka lakini bado kuna vitu alikuwa hajui kama ni kosa hivyo alihitaji
kujifunza zaidi maana kuna mambo bado alikuwanayo.
Toka siku hiyo Edwin
alikuwa mpole sana. Alijiona yeye ni wachini sana kwakuwa kwao hawana pesa.
Alijishusha thamani na furaha yote ilipotea, akawa ni mtu wakujitenga muda wote.
Hali ile ilimshangaza kila mmoja maana
ilikuwa ni ghafla sana kutokea. Editrin pia alishangazwa na badiliko lile na
hata alipomuongelesha Edwin alijibu kwa kifupi sana,
na hakupenda kupiga naye stori kama ilivyokuwa mwanzo.
Editrin alishangaa kwani hakuwa anajua
kuwa yeye ndiye wamwisho kumfanya Edwin akose amani na kubadilika vile maana kwake aliona ilikuwa kawaida tu.
Edwin akawa anajitenga sana na
hata muda wa ibada alikuwa anakaa nyuma na
hata katika
maombi alionekana kuomba kwa
uchungu sana. Licha ya kuwa mwenyekiti lakini, alikuwa hapendi sana hata kusimama
mbele ya watu tena kama mwanzo, hili liliwaumiza wengi na walipomuuliza
hakujibu chochote.
Baada ya wiki mbili kupita Editrin alipewa taarifa
kuwa uamisho umekamilika hivyo siku inayofuata ambayo ni siku ya jumatatu anatakiwa kuondoka shuleni hapo. Ile taarifa ilimuumiza sana
Editrin maana alijikuta hatamani tena kuondoka. Ilipofika usiku
wakiwa prepo Editrin alisimama mbele ya darasa na kuaga darasa kwa kusema kuwa jumatatu ambayo ndiyo siku inayofuata alikuwa anaondoka kuelekea Dar
es salaam ambako ndiko atakuwa anasoma.
Edwin alishangaa sana maana
hakuwa anajua. Editrin alipomaliza kuaga alirudi kukaa kwenye siti yake karibu na Edwin.
"Hivi ni kweli unaondoka?" Alihoji Edwin akiwa haamini.
"Ndiyo"
"Kwanini?"
"Nilishamwambia baba kuwa
nataka kuondoka kwahiyo uhamisho umekamilika. Japo ni
muda kidogo kwahiyo hata mimi nilikwisha sahau".
"Kwanini uondoke?"
"Aa... Hapa sikupapenda tu, japo kwasasa nilitamani kubaki ila sina jinsi tena"
"Anhaa. kwani baba yako
anafanya kazi gani?" Edwin alihoji huku anatazana
taftari lake bila kujua kwanini kauliza.
"Ni mmiliki wa mabasi ya 'A
quality"
"Anhaaa ndiyo maana"
"Ndiyo maana nini?"
"Hivi
mimi na wewe si tunakaa dawati moja, ulishindwa kuniaga mimi kwanza?"
"Sasa unadhani
ningekwambiaje mtu hutaki kuongea na mimi?"
"Editrin wewe unadharau sana, kweli nakwambia. Na usipo jirekebisha
hutofika sehemu salama". Aya basi sawa nenda. Na uwasalimie ukifika" Edwin aliongea vile kwa upole sana na alionesha kuwa anaelewa
vyema anachosema.
"Halafu mbona kama unanichukia
Edwin nilikufanyia nini wewe?"
Aditrin aliuliza akiwa kaumia sana kuitwa mwenye dharau halafu na rafiki yake.
"Hamna kitu. Am
sorry, safari njema Mungu akutangulie". Edwin
alisema hivyo
na kuonyesha tabasamu la kujilazimisha kisha akatoka nje na hakurudi tena.
Siku iliyofuata Editrin aliondoka na
hakuweza kumuona rafiki yake toka usiku ule. Kile
kitu kilimuumiza sana maana Edwin ndiye aliyekuwa
mtu wa karibu sana na kibaya zaidi hata namba ya simu ya Edwin hakuweza
kuipata, maana Edwin alishawahi kusema kuwa hana simu lakini Editrin
alijua ni utani tu.
Alipofika katika shule mpya alianza
kujitahidi kuwa mtu wa ibada na hakuwahi msahau rafiki yake Edwin, licha ya kuwa waliagana vibaya sana. Editrin alijiona kuwa
anabadilika tabia na kuwa mpole, mstaarabu, mwenye heshima, akawa na imani,
lakini pia, akajua kusamehe. Mwisho akawa anajisemea mwenyewe,
"mbona nakuwa na tabia nzuri kama Edwin?, Kwakweli Asante Mungu umenitoa
mbali".
Siku moja alimpigia mwalimu wao wa darasa wa
"Kugilwa high school" na kumweleza kuwa alihitaji kuongea na Edwin.
Mwalimu alimwambia kuwa kwawakati huo Edwin yupo kwenye mtihani ila akitoka
atamwambia kuwa Editrin alihitaji kuongea nae.
Ilipofika jioni mwalimu alimwita Edwin
na kumweleza kuwa Editrin alihitaji kuongea nae. Lakini Edwin
alikataa kwa kusema anaharaka labda wakati mwingine.
Mwalimu alimtafuta Editrin na akamwambia kile Edwin alichojibu. Wakiwa
wanaendelea kuzungumza madam Emily alijikuta
anawiwa kumweleza Editrin kuhusu maisha ya Edwin. Alimwambia kuwa Edwin
ni yatima anaishi na walezi tu ambao ndiyo kama wazazi wake lakini ukweli ni
kuwa walikuwa ni ndugu wa baba yake. Na kifo cha wazazi wake kilitokana na
umaskini maana baba yake alikufa kwa maleria tu lakini kwakuwa
alikosa dawa alipoteza maisha, na mama yake pia
hakuchukua muda akafa. Kwaiyo ni mtoto anayesomeshwa kwa msaada wa shirika la
kiserikali. Madam Emily alimwambia vile Editrin ili kama
angeweza basi amsaidie rafiki yake Edwin kwa chochote.
Baada ya mazungumzo yale Editrin aliumia
sana kwasababu hakujua
hilo kabla na ndipo akajua kwanini Edwin alikosa amani baada ya
yeye kuidharau zawadi aliyopewa. hivyo aliazimia kumsaidia Edwin kwa siri.
Aliongea na mwalimu na akamwambia kuwa
atakuwa anamtumia hela Edwin laki 2 kila mwezi kupitia
simu ya mwalimu lakini Edwin asijue. Mwalimu alifurahi
sana kuona kuwa Editrin ana moyo wa kusaidia
wengine kiasi
kile.
Editrin kweli akawa anatuma hela kila mwezi maana, kwao hela ilikuwa sio tatizo kwasababu kila mtoto
aliwekewa pesa ya kutosha kwenye akaunti ya benk kila mwisho wa mwezi. Edwin
akawa anashangaa hela zile zilitoka wapi,
lakini
mwalimu aliishia kusema mfadhiri wako katuma hela na hakuwahi kumwambia ukweli mpaka
alipomaliza kidato cha sita.
Editrin na Edwin walikuja kukutana tena
chuo kikuu cha "Mzumbe-Mbeya" ambapo
wote walikuwa wakisomea sheria na wakati huu Editrin alikuwa
mtumishi mzuri sana sio kama mwanzo.
Siku walipokutana ilikuwa kama ndoto kwa kila mmoja wao maana
walikutana ibadani wakiwa wanajitambulisha muda wa ibada.
Tokea hapo urafiki wao uliendelea na
Editrin aliweza kuomba msamaha kwa rafiki yake Edwin. Kila mtu aliamua kusahau
yaliyopita. Na wakati huu Edwin alikuwa
kaanzisha mradi wa kufuga kuku wa kisasa kijijini kwao hivyo hakuwa anategemea
misaada tena kwa mtu yeyote.
Walijikuta wakipendana sana na wakaazimia
kuoana pindi wakimaliza masomo.
Baada ya kumaliza mwaka watatu Editrin
alirudi Dar es salaam na akamwambia mama yake Eliana kuhusu kuolewa na Edwin. Mama yake hakuwa na
shida kabisa lakini ilikuwa tofauti sana kwa baba
yake Mr. Edward ambaye alichukia sana baada ya kusikia
taarifa zile na alifoka sana.
Baadaye Editrin aliambiwa kumbe baba yake alikwisha muandaa mtu wa
kumuoa binti yake. Kijana aliyechaguliwa alikuwa ni
mtoto wa familia ya kitajiri iliyokuwa na urafiki na familia yao. Kijana huyo aliitwa Esau.
Editrin hakuwahi kumpenda
hata kidogo kijana huyo hivyo alimweleza mama yake
na kaka yake
kuwa hawezi kukubali kuolewa na Esau ambaye alikuwa ni
kijana kutoka familia ya watu wenye pesa sana. Mr. Edward hakuwahi kumfokea binti yake wala kumlazimisha jambo, hata
baada ya kusikia kuwa binti yake kawa mtu wa dini hakumzuia kabisa kusali bali
alimpongeza tu na akawa anamtania sana kwa kusema Editrin saizi ndiyo kamjua Yesu
kwahiyo anawazidi imani wote mule ndani. Lakini wakati huu, kila mtu
alimshangaa maana alilazimisha kwa nguvu zote ndoa ifungwe.
Mr. Edward aliamua kuandaa harusi ya binti yake kwa lazima jambo ambalo
hata Edger kaka wa Editrin hakulipenda.
Zikiwa zimebaki siku chache harusi kufungwa Edger aliomba namba ya Edwin
kwa Editrin, maana Edger alikuwa anajua kuwa mdogo wake hampendi Esau na
istoshe hata yeye hakuwa anampenda Esau kabisa. Hii ni kwasababu Edger alikuwa
ni rafiki wa Esau na alizijua tabia za rafiki yake. Hivyo, bila kuwa na
wasiwasi alikwishajua namna dada yake atakavyoteseka.
Editrin hakujua kwanini kaka yake kaomba namba ya Edwin. Wakati huo
Edwin alikwisha pewa taarifa kuwa Editrin anaolewa na mtu mwingine na alikuwa amekata
tamaa kabisa.
Siku moja Edwin alipigiwa simu na Edger na kuulizwa kuwa anapatikana
wapi. Hakujua kwanini Edger anamtafuta lakini, kwakuwa Edger alijitambulisha
vizuri kwake kuwa ni kaka yake Editrin, hakuona tatizo kumuelekeza. Edger
alikwenda na gari lake hadi Dodoma-Mpwapwa na alipokelewa na Edwin stendi.
Baada ya kukutana tu Edwin aliingia kwenye gari la Edger na mlango
ukafungwa. Wakiwa ndani ya gari Edger alimuuliza Edwin "unampenda Editrin
kweli?" Swali lile lilimtoa machozi Edwin ambaye alionesha kukata tamaa
lakini alijibu "ndiyo".
Baada ya kujibu tu, Edger aliwasha gari na kuanza kuondoka. Wakati Edwin
anawaza kumuelekeza kwao, Alishangaa gari inawashwa kuelekea lami. Edwin
alishituka sana maana hakujua wapi wanaelekea. Alipouliza, Edger alimjibu acha
uoga kuna jambo la muhimu tunatakiwa kufanya leo kabla siku haijaisha. Edwin
hakuwa amejiandaa kwa safari lakini akaona hana namna ya kukataa.
Walifika hadi Dar es salaam siku hiyo hiyo na ilikuwa ni usiku sana, muda
kama wa saa 7:30 hivi za usiku.
Edwin hakuwai kufika Dar es salaam kwahiyo alikuwa
akishangaa sana na hakujua wako wapi wala wanaenda wapi.
Alipelekwa kwenye duka moja ambapo alikuta kuna suti nzuri imeandaliwa
na akaambiwa avae. Baada ya kuvaa, Edger alimchukua Edwin mpaka mwenye ofisi
moja ambayo ilikuwa imepambwa vizuri mno kana kwamba kuna jambo linaendelea
pale. Walipoingia ndani walimkuta baba mmoja wa makamo kidogo anawasubiri.
Baada ya kuingia Edger alindoka na akamwambia Edwin asubiri pale. Edger alirudu
muda wa saa 9:15 mchana akiwa na Editrin.
Editrin na Edwin hawakuamini kuwa wamekutana tena. Walikumbatiana huku
wakilia, wakiwa hawajui kinachondelea, yule baba aliyekuwepo pale ofisini
alisema waache kupoteza muda. Waligeuka na kumtazama.
Walishangaa vyeti vya ndoa vikiletwa na wakambiwa ni ndoa inatakiwa
kufungwa pale. Editrin hakuamini lakini alifurahi na kumshukuru sana kaka yake
Edger maana aliona hii ndiyo nafasi pekee ya yeye kukwepa ndoa ya lazima kutoka
kwa baba yake.
Kweli ndoa
ilifungwa, na baada ya kufunga ile ndoa ya kiserikali, Edger aliandaa hotel
nzuri sana kwaajili ya shemeji yake Edwin na dada yake na akalipia kwa muda wa
wiki moja. Aliwaambia wasijali kuhusu baba yeye atajua cha kufanya.
Siku iliyofuata Edger alikwenda kwa baba yake na kumwambia kuwa Editrin
amekwisha olewa. Mr. Edward alichanganyikiwa na akaamuru mwanaye Edger apelekwe
polisi.
Editrin hakujua kinachoendelea nyumbani kwao na hakutaka hata kuwasha
simu yake maana Kaka yake alimwambia azime simu kwanza mpaka hasira ya baba
ipungue. Baada ya miezi miwili kupita aliamua kwenda nyumbani kwao kuwasalimia
maana wakati huo alikuwa anaishi na Edwin Dodoma mjini.
Alipofika nyumbani hakumkuta baba yake. Hivyo, alipata muda mrefu sana
wa kuongea na mama yake, ambaye alimueleza mambo yote yaliyotokea, na kwa
wakati huo Edger alikuwa kasha tolewa polisi ila alikuwa Iringa kwenye mambo ya
kazi. Eliana alimwambia editrin kuwa Edger alikuwa anatarajia kuoa siku chache
tu zijazo japo yeye alikuwa anaoa mtoto wakitajiri aliyeitwa Edina. Editrin
alifurahi sana kusikia kaka yake anaoa.
Wakiwa wanaendelea kuzungumza Mr.
Edward aliingia, lakini hakuonesha kushtuka wala kukasirika, bali aliwasalimia
tu na kupita. Editrin aliogopa kidogo hivyo aliaga na kuondoka kurudi Dodoma.
Siku ya harusi ya kaka yake aliamua kwenda na mume wake Edwin kwenye harusi.
Harusi ilikuwa nzuri na yakifahari sana. Usiku walikwenda ukumbini, wakiwa
ukumbini Mr. Edward alikwenda kwa binti yake, na kwa mara ya kwanza aliuliza
"huyu ndiyo mkwe wangu?" Editrin alijibu "ndiyo" akiwa na
hofu sana. Mr. Edward alitabasamu na kusema "karibu sana kijana wangu
nimefurahi kukuona" Kisha akatoa mkono wa karibu kwa Edwin.
Edwin na Editrin walishangaa sana. Edwin kimoyo moyo alimshukuru Mungu
sana. Baada ya harusi kupita walirudi nyumbani kwao Dodoma.
Baada ya mwaka kupita Editrin
alipata mtoto wakiume ambaye alipewa jina la Elvine, Edwin ndiye aliyetoa jina
hilo, na alisema kuwa mwanaye anataka amlee vizuri ili aje kuwa mtumishi mzuri
sana wa Mungu.
Baada ya Editrin kujifungua mtoto huyo, wazazi wa Edwin ndiyo waliokuwa
wa kwanza kuja na kumuuguza Editrin na walimuonesha upendo sana. Baada ya wiki
kupita ndipo wazazi wa Editrin pia walikuja kumsalimia binti yao huku wakiwa na
zawadi nyingi sana.
Baada ya miezi mitatu kupita Edwin aliweza kuajiriwa na serikali kama
mwana sheria wa serikali, lakini hakutaka mkewe afanye kazi. Hivyo, walifungua
duka kubwa la jumla maeneo ya nanenane-Dodoma
Edwin alifanya kazi mwezi mmoja tu, na ndipo Editrin alipopata taarifa
kuwa mumewe amepotea katika mazingira ya kutatanisha. Wakiwa wanaendelea
kumtafuta walipata taarifa kuwa kuna mtu amekutwa kachomwa moto jijini Dar es
salaam karibu na bahari na alikuwa amevaa saa ya Edwin maana sura haikutazamika
kwa namna alivyoungua. Taarifa ile ilithibitisha kuwa aliyekuwa kafariki ni
Edwin tena kwa kuuwawa kikatili.
Editrin alilia sana, hivyo waliuchukua mwili ule na
kuuzika.
Editrin
baada ya kumpoteza mume wake aliamua kurudi nyumbani kwao. Alipokelewa vizuri
tu. Lakini baada ya wiki moja kupita Mr. Edward alisema hahitaji kuona mtoto wa
masikini kwenye nyumba yake hivyo mtoto apelekwe kwenye kituo cha wototo yatima
na yeye aolewe na mtu mwingine ambaye yeye kama baba kamuandaa.
Editrin hakuwa tayari. Hivyo siku ya jumapili alikwenda kanisani na
kutoa nadhiri kwa Mungu kuwa Elvine akikua vyema basi atakuwa ni Mtumishi wa
Mungu, na yupo tayari kwa lolote ila mwanaye hato ruhusu apelekwe kituo cha
watoto yatima. Ni bora hata alelewe na mtu mwingine ila sio kituo cha watoto
yatima kwakuwa mwanaye siyo yatima. Na katika ndoto zake alitamani mtoto huyu
awe na hatima njema na awe msaada kwa wengine. Alimuweka mtoto katika nadhiri
ya kuwa mtumishi katika huduma ya uchungaji kwakuwa alitamani Elvine aje
atimize ndoto za baba yake (Edwin).
Baada ya kurudi nyumbani aligundua kuwa kifo cha mumewe, Edwin, baba
yake ni muhusika na ndiye alipanga mipango yote. Aligundua hili baada ya
kusikia ugomvi kati ya baba yake na mama yake, wakati mama yake akiwa anamlaumu
Mr. Edward kwa kuharibu maisha ya binti aliyemzaa mwenyewe lakini Edward
alisema tu! hayo yameshapita na yeye hajui chochote ila anachotaka ni binti
yake aolewe kiheshima. Jambo hili lilithibitisha kuwa mama yake alikuwa
wakwanza kujua jambo hili, japo aliogopa kumwambia binti yake. Editrin aliumia
sana na ndipo alipoamua kutoroka kwao na kwenda kuishi Iringa. Jambo lile
lilimfanya asimwamini mtu yeyote kutoka kwao. Pia alikumbuka kuwa miaka kadhaa
iliyopita baada ya yeye kuja iringa kaka yake alifanikiwa kufahamu mahali alipo
na alishawishiwa sana na Edger kurudi nyumbani lakini hakuwa tayari kufanya
hivyo. Hivyo alimwambia Edger kuwa asije tena kwake maana hataki mwanaye
ateseke tena na wala hataki kukumbuka yaliopita, kwahiyo toka siku hiyo
hakuonana tena na Edger wala mtu yeyote wa kwao, maana Edger alichukia sana
baada ya kuona msimamo wa mdogo wake kuamua kujitenga hivyo aliondoka na hakuja
tena. Lakini pasipo Editrin kujua, Edger ndiye aliyepigwa jiwe la kichwa na
Elvine ule usiku wakati Elvine alipokuwa anatoka kwa rafiki yake Efraim.
* * *
* * *
* *
Elvine alishituka na akajikuta hospitali. Alishangaa kuona kazungukwa na watu asiowajua kabisa, na cha ajabu zaidi walikuwa ni wachina wanne na mwafrika mmoja. Aliogopa sana kisha akauliza "hapa ni wapi?". Watu wale walionesha tabasamu lililoashiria furaha ya yeye kuamka, lakini walionesha dhahiri kuwa hawakuwa wanamuelewa kabisa anachoongea....
Sehemu ya nne >>>>>Itaendelea jumatatu. Usikose kufatilia.
Kupata mwendelezo wake bofya hapa
Hadithi hii imetungwa na kuandikwa na JACQUELINE JOHN.
Mwimbaji
na mtunzi wa nyimbo, mashairi, Hadithi (simulizi) na ngonjera.
Whatsapno. >>>>>
+255789523850. Normal >>>>>+255747313148.
Mawasiliano:
Whatsapno. >>>>> +255767653697. Normal >>>>>+255783327456.
GeT tO tHe NeXt LeVeL!
Kama umejifunza kitu shiriki nasi katika
comment hapo chini. Ili tupate kujifunza kwa pamoja na kuboresha zaidi.
Sort by: Date Rating Last Activity
Comments by IntenseDebate
Posting anonymously.
Abel Banene · 93 weeks ago
Elias · 93 weeks ago
Abel Banene · 93 weeks ago
Elias · 92 weeks ago
Pearson Sospeter · 92 weeks ago
Hata mm nilipokuwa nasoma A level Mpwapwa Sec nilipewa na zawadi na (.......) nikakataa daah baadae nikajutia. Hivyo zawadi ni zawadi na ni vizuri UKAIPOKEA😪
Lakini pia stori hii ya kuchaguliwa mchumba nimeangalia kwenye Drama moja inaitwa DARLING na kuna vitu vingi nilijifunza kuhusu MAHUSIANO.....
Nimekaa hapa nasubiri Sehemu ya NNE
MTUNZI NA MHARIRI KAZI YENU NI NJEMA
Migongo Elias · 92 weeks ago