HATIMA YA KIMUNGU SEHEMU YA 31
.jpeg)
SIMULIZI
YA KUFURAHISHA, “KUHUSU HATIMA YA KIMUNGU”.
SEHEMU YA SABA.
Ilipoishia.....
Kule
chumbani Elimina aliamua kunywa panado na mseto(dawa za malaria) ambavyo jumla
yake vilikuwa ni vidonge 47. Wakati huku sebuleni maongezi yakiwa yanaendea
mama Elimina aliona aende chumbani kwa binti yake akamfariji, lakini oooh!!
Hakuamini kabisa alichokiona baada ya kuingia chumbani.
Kusoma sehemu ya sita bonyeza hapa
Mama
Elimina hakuamini wala hakufikria kama binti yake angeweza kufanya uamuzi kama
ule. Yule mama alipiga kelele kama aliepatwa na kichaa baada ya kumkuta binti
yake kalala chini huku akitokwa na povu mdomoni.
Kelele zile
ziliwashitua
sana Elvine na mchungaji Moses ambao walikuwa bado katika mazungumzo sebuleni,
baada ya kusikia kelele na wao wakaamua kukimbilia kelele
zilikosikika ili wakajue ni nini kilichotokea. Walipofika hawakuamini kabisa.
Elvine alishituka hadi akaajikuta kaishiwa nguvu, akakaa chini kwasababu ya
uoga maana hakuwaza kama Elimina angekuwa anampenda yeye kiasi kile.
Mchungaji Moses alipoona hali ile alitoka
nje haraka na kwabahati nzuri walikuwa na ng'ombe wawili wa maziwa
hivyo aliwahi kwenda kukamua maziwa na kuja nayo haraka mule chumbani.
Wakati huo mama Elimina alikuwa akilia huku akisema. "Elvine umeniulia
binti yangu".
Elvine alianza kulia huku akitetemeka
maana hakujua hata cha kufanya. Na kwa dakika chache alizokuwa
pale akilia alijikuta kakumbuka namna binti Elimina alivyokuwa mwema kwake toka
walipokutana China. Aliumia sana na akajuta kudanganya
alijisemea tu kimoyo moyo "kwanini mimi lakini, kwanini nimefanya hivi?.
Baba alikuja na maziwa na haraka
akamnywesha binti yake ambaye tayari alikuwa kwenye hali mbaya sana. Elimina hakuwa
mtoto pekee bali alikuwa na kaka zake wawili ambao walikuwa
tayari wanafamilia zao kwahiyo yeye alikuwa ni mtoto pekee wa kike ambaye yupo nyumbani katika ile familia.
Yale maziwa yalikuwa msaada mkubwa sana
maana kidogo Elimina alionekana kama anayerudi kwenye hali ya kawaida.
Elvine wakati akiwa pale mlangoni alipokuwa kasimama alisikia kama mtu
anamnong'oneza kwa sauti ya chini sana "omba uongozwe sara ya toba na
mchungaji Moses".
Alishituka na akageuka pande zote aone ni
nani aliyemwambia vile, lakini hakuona mtu.
Alishangaa sana na akashindwa kusema kwani alikuwa
ameogopa sana maana alijua sio rahisi kueleweka kwa namna
wazazi walivyokuwa
wamechanganyikiwa kuhusu binti yao.
Baadaye Elimina alipelekwa hospitali na
akapewa huduma nzuri zaidi za kimatibabu, lakini hakuweza kuamka.
Walikaa wiki nzima lakini Elimina hakuamka.
Siku moja Elvine alikwenda hospitali peke
yake muda wa jioni kumuona Elimina. Alipofika alishangaa sana kuona wagonjwa
wote wamelala na licha ya kuwa ulikuwa ni muda wa kuona wagonjwa,
lakini hakuna hata mtu mmoja aliyekuja pale hospitali kumtazama mgonjwa wake.
Aliingia kwenye wodi ile
huku akiwa na hofu kidogo maana ule utulivu wa mule ndani ulimtisha kidogo.
Alipofika kwenye kitanda cha Elimina alimkuta Elimina bado hajitambui kabisa.
Ile hali ilimuumiza sana na akajikuta akilia huku akimuomba Elimina msamaha japo
alijua kabisa Elimina hasikii chochote.
Ilikwa saa 12:30 lakini hakuna hata muuguzi
aliyekuja mule ndani. Ghafla Elimina aliamka na kukaa kitako vizuri
pale kitandani. Elvine alishituka maana Elimina aliamka ghafla sana.
Wakati anashangaa akaamua
kumuuliza, "unaendeaje?" Elimina hakujibu bali alikuwa akimtazama tu.
"Elimina nisamehe sana rafiki yangu,
sikujua kama hili litatokea, am really sorry, nisamehe Elimina"
Elvine aliongea kwa uchungu sana.
"Kwanini unalia?" Elimina alimuuliza
kwa upole sana. Ile sauti ilimshitua sana maana haikuwa sauti ya Elimina japo
aliyeongea alikuwa ni Elimina. Lakini hakujali sana maana alihisi labda ni
sauti ya kigonjwa.
"Najua nimekosa kwako hata kwa
Mungu"
"Sasa kwanini hukutii?"
"Sikutii nini?"
"Ulikosea tangu mwanzo, kwahiyo
unatakiwa kurudi kwenye njia, Elvine uliyekusudiwa ni wewe kwanini usitubu kwa
Mungu wako kwanza? Hivi unajua namna Mungu anakuhitaji wewe? Hivi unajua kuwa
umebeba huduma kubwa sana? Hivi unajua unakusudi la
Mungu na jukumu la kutimiza ukiwa duniani? Mungu anakutaka wewe Elvine. Kaombe msamaha maana
wewe ndiyo sababu ya Elimina kuto kuamka maana hukutii sauti ya Mungu ile
siku"
Elvine aliogopa sana, maana katika yote
yaliyoongelewa hakuna alichoelewa zaidi aliishika sentensi ya mwisho "wewe
ndiyo sababu ya Elimina kuto kuamka" maana ilithibitisha kuwa muongeaji
sio Elimina.
Alimuogopa sana Elimina na akaamua kukimbia
kutoka nje. Alipofika mlangoni ndipo akakutana na watu wakiwa wamechelewa sana
kuja kuwaona wagonjwa wao. Elvine hakujali walitoka mbio sana jambo ambalo
liliwashangaza sana watu.
Alifika mahali na akawa amechoka sana,
ghafla alisalimiwa,
"Hey Elvine ni wewe,
unaendeaje kijana wangu?" Ile sentensi iliingia
hadi ndani ya moyo hadi yeye alishangaa maana alijihisi tofauti sana.
"Ooh! Shikamoo, ni wewe kumbe? Za toka sikuile?"
"Marahaba Elvine.
Njema tu!
Vipi mbona kama unaharaka sana?
"Hapana ni kidogo tu"
"Anhaa! Hivi unakaa wapi
kijana wangu?"
"Nakaa hapo tu mbele hata
sio mbali".
"Ok! Nahisi unaswali
kwangu, hebu uliza". Elvine alishangaa sana maana yule baba
alikuwa ndiye aliyekutana naye siku ya kwanza alipofika Tanzania. Kweli alikuwa
anatamani kuuliza swali japo hakujua ni nani atakaye muuliza.
"Oh, ni kweli, umejuaje?"
"Watu wa rohoni hutambuana
rohoni, mimi nakuona kama unahuduma na nguvu kubwa sana ya Mungu, lakini ni
kama wewe hujajua hilo"
"Mmmh! Sielewi hata, mimi
unahuduma gani, kwani naonekanaje?"
"Hivi tangu ukiwa mdogo hujawahi
kufanya tukio la ajabu au lakushangaza?"
"Ajabu kivipi?"
"Kama muujiza hivi"
"Hapana sikumbuki"
"Ok sijui labda kweli
hujawahi, lakini mimi nahisi kama unajukumu la kufanya, haya uliza swali sasa"
"Eti sauti ya Mungu ipoje
na unaijuaje?"
"Swali zuri sana. Mungu
sikuzote huwa hashuki mwenyewe Duniani, bali hutumia watu, vitu na mazingira. Pia tunaijua sauti ya Mungu kwa
uongozi wa Roho mtakatifu"
"Na vipi kama utakutana
na mtu unayejua lakini akatumia sauti ambayo sio yake? Yaweza
kuwa sauti ya Mungu hiyo?"
"Inawezekana maana sikuzote
Mungu hupenda kuonesha upekee wake kutokana na namna anavyopenda yeye, vipi
imekutokea hiyo hali?"
Elvine aliitikia kwa kichwa
"Ooh, unauhakika kuwa hiyo
sauti iliyotumika ni ngeni kwako?".
"Yes! Ok yote ni mapenzi ya
Mungu."
"Halafu samahani baba, wewe
unaitwa nani?"
"Oh! Jina
langu sio muhimu, ila ningependa uniite pacha maana mimi na wewe tunafanana au
niite hata baba."
"Sawa,
vipi kuhusu mtu unayemtafuta umempata?
"Hapana bado sijampata ila najua sio muda nitampata"
"Ni nani kwani?"
"Ni rafiki wa moyo wangu anaitwa Eddy"
"Anhaa! Sawa basi Mungu akusaidie"
"Amina"
Baada ya mazungumzo ya muda mrefu waliagana
kisha Elvine akarejea nyumbani. Elvine toka tukio la Elimina kunywa vidonge
alikuwa akiishi pale ndani kwa woga sana maana hakujua wale wazazi wanawaza
nini juu yake.
Alipofika nyumbani aliingia chumbani kwake
na kulala. Akiwa kalala aliota ndoto. Katika ndoto alisikia akiitwa na
alipoamka alimkuta mdogo wake wa China Elvila, wakati anashangaa mdogo
wake kafikaje Tanzania alimuona Elvila mwingine ambaye alikutana naye akiwa
mtoto lakini cha ajabu bado alikuwa mtoto vilevile.
Yule Elvila wa utotoni mwake akamwambia.
"Unaelewa maana ya hili jambo?"
"Hapana, sasa mimi
ntaelewaje hapa"
"Maana yake ni kuwa hakuna
jambo lisilowezekana kwa Mungu". Akiwa anashangaa mdogo
wake alimuita "kakaaaa". Alishituka kutoka usingizini na ndipo
alipogundua kuwa sauti aliyokuwa akiitumia Elimina ilikuwa ni ya mdogo wake
Elvila wa China. Elvine alimuogopa sana Mungu.
Alitazama saa, ilikuwa ni saa 3:12 usiku
akaona hawezi tena kulala, hivyo akaamka na kutoka sebuleni, ambako alimkuta
baba yake aliamini bado hajalala.
"Baba samahani"
"Usijali kijana wangu, nini
shida?"
"Naomba kuokoka"
"Waoh! Kumbe hujawahi
kuokoka?"
"Ndiyo!
maana huko nilikokuwa wazazi wangu walionilea hawakuwa wanafahamu chochote
kuhusu Mungu."
"Sawa, nimefurahi sana.
Mchungaji Moses alimuongoza sara ya toba Elvine na kisha
akamuombea, lakini alishangaa maana alikuwa akiwiwa kumwombea kuwa Mungu amtumie
Elvine jinsi apendavyo". Baada ya Elvine kuombewa alipata amani sana
na hata alipokwenda kulala, aliota ndoto za kupaa tu mawinguni akiwa na
malaikwa wa zamu.
Asubuhi walipigiwa simu na wakaambiwa
kuwa, Elimina aliamka toka usiku na sasa wanaweza kwenda
kumchukua hospitali. Wazazi walifurahi sana lakini Elvine alizidi kumuogopa
sana Mungu maana alijua kuwa Mungu anamthibitishia kuwa
alihitaji yeye atubu makosa yake. Mchungaji Moses alikwenda hospitali kumchukua
Elimina.
Elimina alipofika tu nyumbani mama yake
alikuwa na hasira sana kwahiyo alimpiga makofi kwa hasira sana huku akimwambia
kwanini amewaaibisha kiasi kile, maana waumini walitamani kujua
sana kwanini Elimina kanywa sumu lakini wazazi walidanganya tu kuwa binti yao
alipokuwa akija Tanzania alipoteza baadhi ya vyeti vyake vya masomo ndiyo maana
akanywa vidonge.
Elimina alilia sana na akaanza kumchukia
sana Elvine.
Siku iliyofuata asubuhi Elvine aliamka
na akawa anamsubiri Elimina aamke ili amsaidie kwenda kumtafuta mama yake.
Labda watapata taarifa yoyote. Elimina alipoamka alimkuta Elvine kakaa sebuleni
anamsubiri yeye. Elimina hakuongea wala kusalimia bali alipita kama hajaona mtu mpaka jikoni na kuanza kuandaa chai. Elvine aliogopa sana
maana kwa muonekano tu wa Elimina ulionesha kabisa hataki mazoea. Alijikaza na
kutuliza moyo.
Muda wa chai ulipofika wote wakaja kunywa
chai. Lakini mchungaji Moses na mkewe waligundua kuwa binti yao hana furaha
kabisa kumuona Elvine mbele yake. Wazazi wakapeana ishara na kujifanya
wameshiba kisha wakaondoka mezani.
Elvine aliona atumie nafasi hiyo kuomba
msamaha.
"Elimina naomba unisamehe sana
please!"
"Kwalipi"?
"Elimina najua unanichukia
lakini mimi nilichukulia kawaida tu maana nilichokuwa nawaza wakati
huo ni kufika Tanzania tu nimwone mama"
"Kwahiyo unasubiri nini
hapa? Si uende kwa mama yako?"
"Elimina nahitaji msaada
wako sana"
"Mmh! Mimi tena?"
"Tafadhari sana, naomba
usinichukie hivyo, tumefundishwa kusamehe sisi kama watoto wa Mungu"
"Nani mtoto wa Mungu? Wewe?"
"Sisi sote"
"Kama na wewe ni mtoto wa
Mungu basi dunia imeisha"
"Elimina please, nisaidie
kumpata mama, pindi nikimpata mama sitakusumbua tena, nakuahidi!"
"Kamtafute mwenyewe, achana
na na maisha yangu kabisa. Elimina baada ya kuongea maneno hayo aliondoka na
kwenda chumbani kwake akamuacha Elvine pale sebuleni akiwa amekosa amani kabisa.
Ulipofika muda wa chakula cha mchana,
Elimina hakuja kula kabisa, na ilipofika jioni
Elimina alikuja lakini hakuinua kichwa kumtazama mtu. Kwa upande wa Elvine naye
alionekana hana amani hivyo naye aliinama tu muda wa chakula wala hakutazama mtu.
Wazazi walikwisha jua kuwa watoto hawa hawana furaha tena.
Siku
iliyofuata asubuhii mchungaji na mkewe waliamua kuwaita na kukaa nao ili
wawapatanishe lakini ikawa ngumu sana. Baadaye wazazi waliamua kumwambia
Elimina amsadie mwenzie kumtafuta mama yake hata kama anamchukia. Kwa
kulazimishwa aliamua kukubali japo sio kwakupenda.
Asubuhi
walijiandaa mpaka mtaa ambao mchungaji Moses aliwaeleza kuwa ndiko mama yake
alipohifadhiwaga baada ya kuchanganyikiwa. Lakini haikuwa rahisi maana
hawakuweza kuipata iyo nyumba maana wengi walikuwa ni wahamiaji wapya katika
mtaa ule hivyo walirudi pasipo mafanikio. Siku iliyofuata walikwenda tena
lakini bado hawakufanikiwa wiki nzima walitafuta lakini hawakuweza kuipata
nyumba hiyo. Walichunguza wiki mbili lakini hawakufanikiwa. Utafutaji wao
ulifanyika kila mmoja akiwa haongei na mwenzie. Njia nzima walikuwa kimya
Elimina kazi yake ilikuwa ni kuongoza njia na Elvine kazi yake ilikuwa ni
kuulizia na kutoa maelezo kuhusu mama yake kwa watu. Jambo hili liliifanya kazi
kuwa ngumu na kuchosha sana.
Mchungaji Moses aliamua kutangaza kanisani kama kuna mtu yeyote anayejua
taarifa za Editrin basi amsadie Elvine. Baada ya ibada mama mmoja alikwenda kwa
mchungaji na akaomba kuonana na Elvine. Elvine aliitwa.
Yule mama alimuuliza Elvine "hunikumbuki mimi?"
"Sina uhakika ila sura yako sio ngeni kwangu"
"Mimi ni mama Efraim"
"Anhaa!! Nimekukumbuka tayari, vipi Efraim yuko wapi?
"Yule mama hakujibu ila alitikisa kichwa tu kuonesha
anasikitika"
"Mbona una...?"
"Efraim alifariki muda sana"
"Hapana, kwanini sasa? Kwanini?"
"Aligongwa na gari"
"Haiwezekani!! Haiwezekani kabisa"
Elvine taarifa zile zilimuhuzunisha sana na alishindwa kujizuia kutoa
machozi, maana Efraim alikuwa ni rafiki yake pekee wa utotoni waliopendana
sana.
Yule mama alimtuliza Elvine kisha akamwambia kuwa yeye ndiye aliyekuwa
akikaa na mama yake baada ya mama yake kuchanganyikiwa lakini kuna mama alikuja
kumchukua na kuondoka naye maana alikuwa ni mama yake Editrin yaani Bibi yake
yeye Elvine.
"Bibi? Mbona mama hakuwahi niambia kuwa tuna ndugu?"
"Mwenyewe hakuwahi niambia lakini hiyo siku ndiyo nilijua. Lakini
pia, nilisikia kaolewa na tajiri mmoja aitwaye Emiliano na ndoa yake ilirushwa
kwenye runinga."
Mmmh! Mama yangu kaolewa kumbe! Natumai anaishi maisha ya raha huko.
Baada ya maongezi hayo. Elvine alimuuliza mchungaji Moses kama anamfahamu
Emiliano. Mchungaji Moses alisema ndiyo anamfamu maana Emiliano ni tajiri
anayefahamika sana. Taarifa zile zilimsaidia sana Elvine. Usiku hakulala
kabisa, alianza kufuatilia mtandaoni kuhusu Emiliano na mwisho alifanikiwa kuiona
ndoa iliyofungwa kati ya mama yake na Emiliano kupitia YouTube. Alilia sana
baada ya kumwona mama yake.
Asubuhi muda wa chakula Elvine aliwashukuru sana familia ya mchungaji kwa
msaada wao, kisha akasema kuwa siku inayofuata ataondoka na kuelekea Dar es
salaam maana amepafahamu mahali ambapo ataweza kumpata mama yake.
"Unaondoka? Umepafahamuje kwa mama yako? Na mbona mimi sina taarifa?"
Elimina alihoji kwa mshangao.
!" We shida yako ni nini? We si ulisema hutaki kumwona kijana wa
watu hapa? Mwache aondoke kwa amani sasa, ni kweli alikosea tena sana lakini si
kaomba msamaha, hata yeye alikuwa na matatizo ndiyo maana akakutumia
wewe". Aliongea mchungaji Moses kwa upole tu.
"Ooh! Kumbe wote mpo upande wake haya sawa" Elimina aliondoka
pale mezani na kwenda chumbani. Mama yake Elimina alikuwa akiwatazama tu wala
hakusema neno. Baada ya Elimina kuondoka yule mama akaanza kucheka. Alipoulizwa
anacheka nini alisema hamna kitu.
Ilipofika saa 4:30 usiku Elvine akawa anapanga nguo zake ili kesho aanze
safari lakini alishangaa kuona Elimina akimtumia "safari njema".
Hakuamini maana haijawahi tokea toka afike pale ndani kupokea sms ya Elimina.
Alitabasamu na akajibu "Asante sana, uko wapi nataka nikuage"
"Nipo nje!" Elimina alijibu
Elvine alifurahi sana, akatoka nje na kumkuta Elimina kakaa kwenye kiti.
"Mbona upo nje usiku wote huu?"
"Nimekaa tu"
"Ooh! Sio salama kwa afya yako."
"We ni nani hata unihofie mimi"
"Samahani"
"Never mind"
"Ok, nisamehe kwa kila kitu pia nimekusamehe, halafu kuhusu ile
siku sitoikumbuka tena"
Elimina alijikuta katabasamu na akakumbuka kuwa kuna siku alimtelekeza
Elvine mtaani wakati wanamtafuta Editrin kwahiyo Elvine alipotea akatangatanga
sana mtaani, Elimina alirudi nyumbani usiku lakini hakumkuta Elimina
alipoulizwa Elvine yuko wapi alidanganya kuwa kamuacha mahali kuna kitu
anafanya. Kwahiyo ikabidi arudi kumtafuta na alimkuta Elvine kakaa mahali hajui
hata aende wapi.
Walipokumbuka hili wote walicheka. Wakati huo kumbe mama alikuwa mbele
yao. Akawauliza "nyie maadui wawili mnafanya nini sasa hivi hapa nje na
usiku wote huu?"
Walishituka sana na wakawa wanawaza namna ya kujitetea...
Sehemu ya nane itaendelea jumatano
>>>>>. Usikose kufuatilia.
Kupata mwendelezo wake bonyeza hapa
Hadithi
hii imendaliwa na kuandikwa na JACQUELINE JOHN.
Mwimbaji
na mtunzi wa nyimbo, mashairi, Hadithi (simulizi) na ngonjera.
Mawasiliano:
Whatsapno.
>>>>> +255789523850. Normal >>>>>+255747313148.
Na,
Imehaririwa
na MIGONGO ELIAS. Mhariri.
Mawasiliano:
Whatsapno.
>>>>> +255767653697. Normal >>>>>+255783327456.
GeT tO tHe NeXt LeVeL!
Kama
umejifunza kitu shiriki nasi katika comment hapo chini, ili kujifunza na
kuboresha zaidi.